Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kamishna wa Kaunti ya Kisii Chege Mwangi amewaomba wahudumu wa matatu kuwa waangalifu ili kupunguza visa vya ajali.

Mwangi alisema kuwa waendeshaji magari wengi huendesha magari yao kwa kasi jambo ambalo limepelekea kuongezeka kwa ajali barabarani.

Akizungumza siku ya Jumatano katika eneo la Ogembo, Mwangi aliwaomba madereva kupunguza mwendo wanapoendeleza biashara zao za uchukuzi ili kulinda maisha ya binadamu, haswa msimu huu wa likozi.

Aidha, aliwaomba madereva kuwa makini ili kupunguza visa vya ajali vinanyoendelea kushuhudiwa ili wananchi waweze kuvuka mwaka mpya bila tatizo lolote.

Mwangi aidha aliwaonya madereva dhidi ya kiuka sheria za barabarani kwa kusema watachukuliwa hatua kali za kisheria kwani kukiuka kanuni hizo ni kinyume cha sheria.

Mwangi pia aliomba waendeshaji pikipiki kufuata na kuzingatia sheria za barabarani ili kuzuia kuhusika katika ajali.

“Naomba wahudumu wa matatu na waendeshaji pikipiki kufanya shughuli zao za uchukuzi kwa makini ili kupunguza ajali barabarani,” alisema Mwangi

Aliongeza, “Wahudumu ambao watakiuka sheria za barabarani watachukuliwa hatua na kupigwa marufuku kuendesha magari ya umma.”