Wafanyibiashara wanaofanya shughuli zao kando kando mwa barabara kuu ya kutoka Nairobi kuelekea Mombasa wamewalaumu madereva wa malori ya kubeba mizigo kwa kuyaendesha magari yao kiholela na kupuuza sheria za trafiki.
Haya yanajiri baada ya ajali kutokea katika eneo la Bonje, ambapo watu wasita walifariki huku wengine wakijehuriwa.
Wakiongea katika eneo la Bonje huko Mazeras siku ya Jumamosi, wakazi hao walishtumu vikali madereva na kusema kuwa mara kwa mara wamekuwa wakiendesha malori yao kwa kasi na kuwadharau wenye magari madogo.
Kulingana na Samuel Mwasame, ambaye ni dereva wa gari la abiria linalohudumu katika barabara hiyo kutoka Mombasa kuelekea Voi, madereva wa malori hupenda kuendesha magari yao kwa kiburi na huwazuia wenye magari madogo kuwapita, na kuendesha malori hayo katikati mwa barabara.
“Ni wajibu wa maafisa wa idara ya trafiki kuamka na kuanza kuwakabili madereva wa malori kwa kuwa inaonekana ndio wanasababisha ajali katika barabara hii. Ajali kama hii haingetokea kamwe,” alisema Mwasame.
Polycap Makau, ambaye aliongea kwa niaba ya wakazi alitishia kuchukua hatu ya kuandamana na wakazi wa eneo hilo iwapo madereva hao hawatachukuliwa hatua za kisheria haraka iwezekanavyo.
Afisa mkuu wa polisi katika eneo hilo la Mariakani Patrice Ndeiywa alisema kuwa bado wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na ajali hiyo, huku akisema waliojeruhiwa tayari wamepelekwa Hospitali kuu ya Pwani kwa matibabu na wengine katika Hospitali ya Mariakani.
Barabara kuu ya Nairobi-Mombasa imekuwa ikishuhudia visa vya ajali ambazo mara nyingi zimetajwa kusababishwa na magari ya mizigo ambayo hutoka na kuelekea bandarini kupakia shehena.