Baadhi ya madereva wa magari ya uchukuzi mjini wamewalaumu wamiliki wa magari hayo kwa kukosa kuungana pamoja na kupinga agizo la idara ya uchukuzi la kuyaondoa barabara magari yaliyotiwa nakshi.
Madereva hao walisema kuwa hatua hiyo inarudisha nyuma biashara hiyo na kushangazwa na jinsi wamiliki wa matatu walivyolinyamazia suala hilo licha ya kwamba wao ndio wanaoathirika zaidi.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, dereva mmoja anayeendesha matatu ya kutoka Likoni Ferry kuelekea katikati mwa jiji alisema kuwa wamiliki hao ni waoga na wasio na muungano dhabiti.
“Jambo kama hili linapotokea ni jukumu lao kuungana na kutoa kilio chao kwa idara hiyo kwa sababu haya ni maonevu na inashangaza kwamba hatuelewi sekta ya uchukuzi inaelekea wapi,” alisema dereva huyo.
Wakati uo huo madereva hao pia walisema Rais Uhuru Kenyatta aliwahi kusema kuwa hatua ya kuchora picha katika magari sio tatizo na kwamba wenye nia ya kufanya hivyo wako huru.
“Rais mwenye,we alisema hakuna tatizo kuchora magari lakini baadaye mambo yakageuka, mimi naona basi ni kama mtego tulikuwa tumewekewa ili tuje tukamatwe,” aliongeza dereva mwenzake.
Hapo awali idara ya uchukuzi ilitoa agizo la kukamatwa kwa magari yote yenye michoro isiyo ya heshima na inayopotosha maadili, huku pia ikiongeza kwamba baadhi ya michoro hiyo inazuwia madereva na abiria kuona nje.
Madereva wengi pamoja na wamiliki wa gari za uchukuzi nchini walionekana kupinga vikali agizo hilo huku wakidai kwamba michoro haiwezi kivyovyote kusababisha ajali barabarani wakisema kwamba hiyo ni njama tu ya kuwakandamiza kibiashara.