Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Madereva wa malori wanaotumia barabara ya Salgaa kusafirisha mizigo wametakiwa kuwa waangalifu wanapotumia barabara hiyo ili kuzuia ajali ambazo hutokea mara kwa mara.

Akizungumza kwenye eneo la Kikapu katika kaunti ndogo ya Njoro siku ya Jumanne, mwakilishi wa wanawake kwenye Kaunti ya Nakuru Mary Mbugua, aliwataka madereva kuwa waangalifu hasaa wanapofika kwenye mteremko ulioko katika barabara hiyo.

Mbugua alitoa onyo hilo huku akiomboleza na familia iliyompoteza mtoto wao, Dominic Mwangi, kwenye ajali ya barabarani iliyohusisha vijana watano katika eneo la Salgaa mkesha wa mwaka mpya.

Mwakilishi huyo aidha amewataka wazazi kutoka Kaunti ya Nakuru na nchini Kenya kwa jumla kutowaruhusu wanao wasio na leseni kuendesha magari yao.

Pamoja na hayo, alisema kwamba yeye kama mmoja wa wanachama wa kamati ya kawi katika bunge la kitaifa, amezuru barabara hiyo ya Salgaa na kuhakikisha kwamba ina ishara za barabarani na matuta.

“Ningependa kuwaonya wanaong’oa ishara hizo za barabarani ili kutumia vifaa vinavyotumiwa kutengeza ishara hizo kwa matumizi yao ya nyumbani,” alisema Mbuga.

Aidha, alihimiza serikali kujenga eneo la kuegesha malori katika eneo la Kinungi, ili kuzuia madereva wa malori hayo kusafiri usiku hadi eneo la Salgaa kuyaegesha.

Isitoshe, amewataka wazazi kuwashauri wanao huku akiangazia tukio ambalo lilipelekea vijana hao watano kuaga akisema walikuwa wamebugia pombe kabla ya kuhusika katika ajali hiyo.

Mbugua alisema ushauri huo unafaa pia kujumuisha watoto wote na haswaa wale wa kike ambao hujihusisha na ndoa za mapema.