Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku shule zinapofunguliwa jumatatu kwa muhula wa kwanza mwaka huu, kamishna wa kaunti ya Nyamira Josphine Onunga amewahimiza madereva wa magari kuwa waangalifu barabarani. 

Akihutubia wanahabari katika mkahawa mmoja mjini Nyamira wakati wa mkesha wakuukaribisha mwaka mpya wa 2016, Onunga alionya kwamba madereva ambao hawatazingatia sheria za barabarani watachukuliwa hatua kali za kisheria. 

"Shule zinapofunguliwa, tunatarajia abiria barabarani watakuwa wengi kuliko siku za kawaida na ni onyo langu kwa madereva watakaopatikana wakiendesha magari yao bila kuzingatia sheria za barabarani kuwa watachukuliwa hatua kali," alisema Onunga. 

Kamishna huyo aidha aliwahimiza wasafiri kuwa waangalifu dhidi ya matapeli na wezi ambao huenda wakawapora mali yao wanaposafiri kwenye magari ya umma huku akihimiza kampuni za usafiri kutoongeza nauli za usafiri msimu huu.

"Kufuatia shughuli za usafiri kuendelea kuchacha, kuna baadhi ya watu watakaodai eti wao ni wasafiri ilhali nia yao ni kupora watu mali na bidhaa zao wakati huu na ni himizo langu kwa wasafiri kuwa waangalifu zaidi dhidi ya watu wenye tabia kama hizo na pia ni himizo langu kwa kampuni za usafiri kutoongeza nauli mara dufu kufuatia hatua ya watu wengi kusafiri msimu huu," alihoji Onung'a.