Seneta wa Mombasa Hassan Omar ameeleza imani yake kuwa magavana wengi nchini watashindwa kuvitetea viti vyao katika uchaguzi mkuu ujao, kwa kile alichokitaja kama utepetevu na kutowajibika ipasavyo miongoni mwa viongozi hao wa kaunti.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne katika kongamano la wabunge wa kaunti, Omar, ambaye tayari ametangaza azma yake ya kuwanaia kiti cha ugavana wa Mombasa katika uchaguzi wa 2017, alidai kuwa magavana wengi nchini wameshindwa kuitekeleza miradi ya maendeleo na badala yake wanatumia vibaya pesa ambazo zimetengwa kuufanikisha ugatuzi.
“Kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita ambapo wabunge wengi walivipoteza viti vyao, magavana pia wajiandae kutumwa nyumbani katika uchaguzi ujao,” alisema Omar.
Aidha, Omar aliwahimiza wawakilishi wadi kuhakikisha kuwa sheria wanazopitisha katika mabunge ya kaunti zinawafaidi wananchi badala ya watu binafsi wanaolenga kujinufaisha kwa kuwanyanyasa wasio na usemi katika jamii.
Senata huyo vilevile alisisitiza kuwa licha ya yeye na Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho kuwa katika mrengo mmoja wa Cord, ataugombania wadhifa wa ugavana wa kaunti hiyo katika uchaguzi wa 2017, huku akiwataka wakosoaji wake kuwapa nafasi wapiga kura ili waamue kiongozi wanayemtaka.