Maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Uratibu wa Mipaka (IEBC) imewataka maafisa wa polisi kuyakabili magenge ya kihalifu yanayowahangaisha maafisa wake katika vituo vya usajili wa wapiga kura.
Mshirikishi mkuu watume hiyo katika kanda ya Pwani Kusini Amina Soud amesema kuwa baadhi ya maeneo ya vituo vya usajili wa wapiga kura hususan katika eneo hilo yameshuhudia magenge ya kihalifu yakiwafurusha maafisa wa tume hiyo.
Amesema kuwa baadhi ya maafisa hao wamesema kuwa magenge hayo ya kihalifu hujitambulisha kama wafuasi wa Kundi lililoharamishwa la Mombasa Republican Council (MRC) na hatua hiyo imewatia hofu maafisa wa IEBC pamoja na wakaazi wa maeneo hayo.
“Tumepata ripoti kutoka katika vituo vya usajili kuwa maafisa wetu pamoja na wapiga kura wamekuwa wakihangaishwa na magenge ya kihalifu yanayojitambulisha kama wafuasi wa MRC," alisema Soud.
"Mengenge hayo pia yanawafurusha watu hali ambayo huenda itapelekea kusajiliwa kwa asilimia ndogo sana ya wapiga kura,” aliongeza kusema Sudi.
Amesema kuwa ikiwa hali hiyo itaendelea basi zoezi hilo halitakuwa na manufaa yoyote kwa Wakenya wa ukanda wa Pwani Kusini.