Mahakama ya juu nchini imetupilia mbali ombi la Tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC, la kutaka kubadili agizo lililotolewa na mahakama ya rufaa kwa tume hiyo kulipa walimu elfu 52 waliostaafu mwaka wa 1997 shilingi bilioni 42.3.
Kupitia kwa uamuzi uliotolewa siku ya Alhamisi na majaji wa mahakama hiyo Mohammed Ibrahim, Jacton Ojwang, Smokin Wanjala na Njoki Ndung'u, tume hiyo ya TSC pia imeelekezwa kugharamia kesi hiyo.
Majaji hao walidinda kukubali ombi la TSC la kuitaka mahakama hiyo kutoa agizo la kupinga uamuzi uliotolewa na mahakama ya rufaa mwaka wa 2009 na mahakama kuu ya Nakuru mwaka wa 2006, maamuzi ambayo yalipelekea walimu hao kushinda kesi hiyo dhidi ya TSC.
Katika uamuzi uliotolewa mwaka wa 2006 na jaji David Maraga mjini Nakuru, mahakama ya Nakuru iliagiza TSC kuwalipa walimu hao, huku rufaa ya TSC kupinga uamuzi huo ikitupiliwa mbali Mei 23, 2014.
Akionyesha kuridhishwa kwake na uamuzi huo, Wakili Dominic Kimatta aliyekuwa akiwawakilisha walimu hao alihimiza Tume ya TSC kufuata agizo hilo la mahakama haraka iwezekanavyo, ikizingatiwa kuwa mahakama kuu ilikuwa imetoa agizo la kufungwa jela lwa afisa mkuu wa TSC iwapo agizo hilo halingetekelezwa.
Akizungumza na wanahabari mjini Nakuru, Kimatta alisema Tume ya TSC haina lingine la kufanya kisheria kwani imetumia mahakama zote zilizo Kenya ambazo zimeagiza tume hiyo kuwalipa walimu hao.
Alisema kwa kuwa zaidi ya walimu 800 waliostaafu wamefariki kabla ya kupokea malipo hayo, na kwamba waliosalia wanaugua huku wengine wakitatizika kujitosheleza maishani.
Kimatta aidha ameongeza kuwa jumla ya shilingi bilioni 16.7 zilitengwa kwenye makadirio matatu ya bajeti ili kuwalipa walimu hao lakini walimu hao hawajalipwa kufikia sasa.
Amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kushughulikia swala hilo kwa dharura ikizingatiwa kuwa tayari fedha hizo zilikuwa zimetengwa wakati alipokuwa waziri wa fedha.