Makahama ya rufaa imetupilia mbali rufaa ya kupewa dhamana mshukiwa mkuu wa ulanguzi wa pembe za ndovu Feisal Mohamed.
Wakitoa uamuzi huo siku ya Ijumaa, majaji watu katika mahakama ya Mombasa, wakiongozwa na jaji Asike Makhandia wamesema kuwa rufaa hiyo haina msingi wowote, na kusisitiza kuwa mshukiwa huyo atasalia ndani hadi kesi yake kutamatika.
Haya yanajiri baada ya mshukiwa huyo kupitia wakili wake Pascal Nabwana kukata rufaa hiyo kupinga uamuzi wa mahakama kuu wa kufutilia mbali dhmana ya mteja wake.
Mwezi Agosti mwaka huu, jaji Martin Muya alifutilia mbali dhamana hiyo kwa kusema mahakama ya chini haina uwezo wa kubadilisha uamuzi wa mahakama kuu kwa mujibu wa katiba.
Hii ni baada ya mahakama ya chini kumpa dhamana ya shilingi milioni 10 mshukiwa huyo, licha ya upande wa serikali kupinga jambo hilo.
Mohamed na wenziwe wanakabiliwa na ulanguzi wa pembe za ndovu 314.