Mbunge wa Lamu Magharibi Julius Ndegwa amepata pigo baada ya mahakama ya Mombasa kudinda kutupilia mbali kesi ya ufisadi inayomkabili.
Akitoa uamuzi huo siku ya Alhamisi, Hakimu Julius Nang’ea alisema kuwa tume ya EACC bado inatambulika kikatiba licha ya makamishina wake kujiuzulu.
Aidha, aliongeza kuwa mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma yuko na uwezo wa kuendesha kesi za ufisadi kwa mujibu wa katiba ya nchi.
Haya yanajiri baada ya wakili Danson Mungatana, kuitaka mahakama kufutilia mbali kesi ya ufisadi inayomkabili mbunge huyo tarehe Julai 23, 2015, hadi pale tume ya kukabiliana na ufisadi itakapofanyiwa marekebisho baada ya baadhi ya makamishna wake kujiuzulu.
Mungatana alisisitiza kuwa EACC kwa sasa haitambuliki kikatiba kwa sababu ya mapengo ya uongozi.
Vilevile, aliongeza kuwa mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma hausiki kikatiba katika kuendesha kesi za ufisadi mahakamani.
Madai hayo yalipingwa na naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa, Alexendra Muteti, kwa kusema kuwa madai hayo hayana msingi wowote na kusisitiza kuwa katiba inaruhusu afisi ya mkurugenzi mkuu wamashtaka ya umma kuendesha kesi za ufisadi kwa ushirikiano na tume ya EACC.
Mbunge huyo na wanakamati sita wa hazina ya ustawishaji wa maeneo bunge CDF wanadaiwa kufuja Sh1.6m zilizokuwa zimetengewa ujenzi wa kituo cha kutibu mifugo eneo la Witu.
Kesi hiyo itasikizwa Disemba 10, 2015.