Afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma imepata pigo baada ya mahakama kutupilia mbali ombi la kutaka kesi ya ulanguzi wa pembe za ndovu zilizonashwa nchini Thailand na Singapore kuahirishwa kwa muda wa miezi mitatu.
Akitoa uamuzi huo Hakimu Henry Rotich alisema kuwa afisi hiyo inajikokota katika kuendesha kesi hiyo bila sababu mwafaka.
Hii ni baada ya naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa, Alexendra Muteti, kuwasilisha ombili hilo, siku ya Jumanne kwa kile alichodai kuwa bado pembe hizo ziko nchini Thailand na Singapore, hivyo basi itakuwa vigumu kesi hiyo kuendelea ikizingatiwa kuwa huo ndio ushahidi pekee.
“Bado pembe hizo ziko nchini Thailand na Singapore. Afisi yetu inapata changamoto kuendesha kesi bila kuwepo kwa pembe hizo kwani ndio ushahidi mkubwa katika kesi hii,” alisema Muteti.
Aidha, Muteti aliaongeza kuwa wameziandikia barua nchi hizo mbili ili kuharakisha kusafirishwa kwa pembe hizo hadi nchini Kenya ili kutumika kama ushahidi.
Ombi hilo lilipingwa vikali na mawakili wa washitakiwa, wakiongozwa na wakili Gikandi Ngibuini, kwa kusema kuwa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma haiwajibiki vilivyo katika kuendesha kesi hiyo kwa haraka ili haki na usawa upatikane kwa wateja wao.
Hakimu Rotich aliagiza afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma kujizatiti katika kutafuta pembe hizo ili kuharakisha kusikilizwa kwa kesi hiyo tarehe Januari 20, 21 na 23, 2016.
Kati ya Machi 15 na April 26, karani wa shirika la ulipaji ushuru KRA Lucy Kahoto pamoja na wengine wanane wanadaiwa kuhusika katika ulanguzi wa pembe 511 zenye thamani ya Sh576m.
Kufikia sasa washtakiwa tisa wametiwa mbaroni.