Wakazi wanaomiliki majumba ya kibiashara katika barabara ya Changamwe kuelekea uwanja wa ndege wa Moi mjini Mombasa wametakiwa kuyabomoa majumba hayo ili kupeana nafasi ya upanuzi wa barabara.
Mwenyekiti wa tume ya Kitaifa ya ardhi Dkt Mohammed Swazuri, alisema kuwa licha ya baadhi yao kutahadharishwa na hata kufidiwa ili kuondoka katika maeneo yao, wamekaidi amri hiyo na kuchelewesha ujenzi huo.
Akizungumza wakati alipokagua barabara hiyo akiandamana na Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki siku ya Ijumaa mjini Mombasa, Swazuri alisema kuwa ni lazima nyumba hizo za kibiashara na zile za makaazi zibomolewe.
“Tunawaomba wafanyibiashara na wamiliki wa majumba hayo kuyabomoa mara moja kwa sababu tumejadiliana nao na tumewalipa fidia. Tunashindwa kwa nini wanakaidi amri hiyo na nadhani itatulazimu tuchukue sheria na kuwahamisha ili shughuli za upanuzi wa barabara hiyo kuendelea kutekelezwa,” alisema Swazuri.
Swazuri alisema kuwa wahandisi wanaotekeleza ujenzi huo wamekuwa wakilalamikia vikwazo kutoka kwa wale waliyojenga nyumba zao pambizoni mwa barabara hiyo bila idhini.
Alisema kuwa ni lazima wakazi hao wazingatie amri ya kuhama maeneo hayo.
Tayari mamlaka ya barabara kuu nchini imetenga kima cha shilingi bilioni 4.2 kutumika katika upanuzi wa ujenzi wa barabara hiyo.