Share news tips with us here at Hivisasa

Ongezeko la maambukizi mapya ya virusi vya HIV katika kaunti ya Nakuru limelaumiwa kwa uwepo wa makahaba wengi wanaoshiriki biashara ya ngono katika barabara kuu ya Nairobi-Nakuru-Eldoret.

Kulingana na mshirikishi wa baraza la kupambana na maambukizi ya ukimwi kanda ya bonde la ufa Hillary Chepsiror, ongezeko la shuguli za biashara ya ngono na ukahaba katika miji ya Gilgil, Maimahiu, Nakuru, Salgaa na maeneo mengine umepelekea kuongezeka kwa maambukizi ya HIV licha ya juhudi zinazofanywa kukabiliana na janga hilo.

Akihutubu Jumanne wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya ukimwi ulimwenguni Chepsiror alisema kuwa makahaba wengi hushiriki mapenzi na madereva wa lori za masafa marefu bila kutumia kinga na hiyo inasababisha ongezeko la maambukizi mpya.

“Kaunti ya Nakuru inajulikana kwa biashara ya ukahaba haswa katika barabara kuu ya Nairobi-Eldoret na hii inawajumuisha madereva wa masafa marefu wanaopiga kambi katika vituo vya kibiashara na kushiriki ngono na makahaba bila kinga,” alisema Chepsiror.

“Makahaba wengi huwa hawachukui hatua ya kupimwa kujua hali yao na hata wale wanojua hali zao huwa hawana hofu ya kueneza virusi hivyo kwa wengine,” aliongeza.

Chepsiror alisema kuwa inasikitisha kuwa kaunti ya Nakuru inaongoza kwa visa vya maambukizi mapya ya virusi vya HIV licha ya juhudi kubwa kufanywa kukabiliana na janga hilo.

“Wakazi wengi wa Nakuru hawajui hali yao ya HIV kwa kuwa wanaogopa kwenda kupimwa. Hii imekuwa kikwazo kwa vita dhidi ya HIV,” Chepsiror alisema.