Kulingana na katiba, kaunti ya Nakuru ni nambari 32, na sio hili tu ambalo huifanya isalie katika ramani ya Kenya na ulimwengu.
Katika pita pita zako mjini Nakuru au katika miji ya Naivasha, Subukia, Molo, Njoro na Mau Narok kati ya maeneo mengine, utagundua mambo yafuatayo ambayo ni ya kipekee katika kaunti hii.
Kaunti ya Nakuru imekuwa ikivutia wawekezaji wengi kama sumaku (magnet) kutokana na mwingiliano wa makabila yote ya Kenya ambayo yanapatikana katika mji wa Nakuru, huenda kitu kinachoipa sifa ya kuitwa 'The heart of Kenya'.
Ni katika kaunti ya Nakuru pekee ambako kupata ufuasi wa kisiasa ama kidini ni rahisi kuliko kunywa maji. Tangaza wakati mmoja unafanya mkutano wa kisiasa, na uwe wewe ni kigogo hata asiye na ufuasi, siku hiyo utapata wafuasi ambao wengi watakuwa mabroka wa siasa, au wanaomezea mate utakachotoa baada ya mkutano.
Upate kazi katika kaunti ya Nakuru, usitie wasiwasi kama mfuko wako umetoboka. Kusafiri mjini kutoka mitaa ya mabanda viungani mwa mji wa Nakuru, ni shilingi 30 pekee na vile vile unaweza kutembea kwa miguu…maarufu miongoni mwa wanafunzi kama Using Route eleven. Je unaweza linganisha gharama hii na jijini Nairobi, Mombasa ama kisumu? Ndio maana Nakuru ni ya kipekee.
Kuna uwezekano kila mwanabiashara katika mji wa Nakuru anajua mwenzake, kwani mji huu si mkubwa sana. Kutoka kona moja hadi nyingine ya mji huu, utalipa boda boda shilingi hamsini tu. Lakini hili pia halijazuia majumba makubwa kujengwa, shule nyingi kufunguliwa, vilabu vya kiajabu ajabu vinavyofurika wanafunzi wa vyuo vikuu kufunguliwa, ama biashara isiyo halali ya ngono kuendelea.
Nakuru ni ya kipekee, maduka hufungwa mapema mwendo wa saa moja, ikizidi saa mbili Town Service zikivuna pakubwa kwenye Jam ambayo huchangiwa na mvua. Lakini sio kumaanisha vilabu hukoma kuuza, kwani huo ndio wakati wao wa kuchuma kutoka kwa vijizee vinavyojiburudisha na malaika wadogo haswa wa vyuo, au kikundi kingine cha wanaosema ‘Kazi ni kazi,’ hata ‘My dress my choice’ ni kazi.
Nao wana boda boda hawachoki, usiku wote huo wao huvumilia baridi. Ukiuliza watu wa Naivasha kuhusu hifadhi ya kitaifa ya Hells Gate, watakujibu yote kuihusu wakionekana kutabasamu. Kwa upole watasema, ‘Nilienda tukiwa sekondari na nikaoga kwenye ‘hot shower’ hapo karibu na “devils kitchen".
Ati devils kitchen?
‘Naam, kuna hata devils shower na devils bedroom,’ atakujibu ukishangaa. Katika eneo ambalo si mbali na hapo, sasa kuna Gates of Heaven. Lo! Kweli Nakuru ni ya kipekee
Ukitaka kujua mengi kuhusu mapango ya kiajabu, tembea Menengai crater na Njoro, yote katika kaunti hii.
Ukitaka kuona korongo wanaovutia, jua wanapatikana ziwani Nakuru.
Nakuru hulishwa na maeneo ya Mau Narok, Dundori na Subukia, ambapo chakula huuzwa kwa bei rahisi, hata ukiwa na 20 bob, utashiba.
Utagundua Nakuru kweli ni ya kipekee, ukienda kukwea milima kwenye mbuga hilo la Hells Gate.