Mshirikishi mkuu wa polisi katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa amesema kuwa polisi mjini Mombasa wanalemaza shughuli ya kuchunguza na kuwakamata wahalifu waliosababisha vurugu na kujeruhi watu wakati wa mkutano wa Rais Uhuru Kenyatta mapema mwezi Januari.
Mkuu huyo wa polisi alisema kuwa polisi mjini humo wameshindwa kutekeleza uchunguzi huo kutoka na kile alichotaja kama kuogopa watu fulani.
Mapema mwezi Januari wakati Rais Kenyatta alipokuwa akizindua mradi wa 'Mwangaza Mitaani' katika uwanja wa Makadara, baadhi ya watu walianzisha vurugu ambapo mwanamume mmoja aliripotiwa kuuawa huku wengine wakijeruhiwa viabaya.
Akizungumza na wanahabari mjini humo siku ya Jumatatu, Marwa aliwataka polisi kuharakisha uchunguzi huo mara moja ili washukiwa wa tukio hilo kutiwa mbaroni.
“Tangu tukio hilo kufanyika polisi hawajafanya lolote. Sheria lazima ifanye kazi pande zote. Kwani ni nani huyo mnayemuogopa aliyewazuia nyinyi kutekeleza kazi?” aliuliza Marwa.
Aidha, kamishna huyo aliongeza kuwa kila Mkenya anafaa kupata haki kisheria na kuonya kuwa hakuna mtu aliye na mamlaka juu ya mwingine.
Wakati huo huo, Marwa alitoa onyo kali dhidi ya vijana wanaolipwa kusababisha vurugu wakati wa mikutano, na kuongeza kuwa hali hiyo inarudisha nyuma maendeleo.
“Vijana wanapewa pesa ili wafanye vurugu na hiyo pia hatuwezi kukubali. Sisi tunataka maendeleo na sio matukio ya kuturudisha nyuma,” alisema Marwa.