Kesi ya uchochezi inayomkabili mwakilishi wa wanawake kaunti ya Mombasa Mishi Mboko ilihairishwa tena kwa mara ya pili baada ya mashahidi kukosa kuhudhuria kikao cha kesi kwa kile wanachodai kutishiwa maisha na kuhofia usalama wao.
Haya ni kutokana na mwendesha mashtaka Nicolas Kitonga kutoka afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa.
Kitonga aliomba mahakama siku ya Jumatano kuwaruhusu mashahidi hao kutoa ushahidi wao faraghani ili kulinda usalama wa mashahidi hao.
Aidha, Kitonga aliitaka mahakama kuahirisha kesi hiyo ili afisi yake kuelekea katika mahakama kuu ili kuomba usalama wa mashidi wake chini ya kitengo cha kulinda usalama wa mashahidi.
Jambo hilo lilipingwa na wakili Gerad Magolo, aliyesisiteza kuwa kesi inayomkabili mteja wake lazima isikilizwe hadharani ikizingatiwa yeye ni kiongozi wa umma na mwanasiasa, hivyo basi wafuasi wake wanahitaji kusikiliza ushahidi utakaotolewa dhidi ya kiongozi wao.
Kulingana na naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka Alexander Muteti, mnamo Juni mosi mwaka jana katika uwanja wa michezo jijini mombasa, mwakilishi huyo alisema maneno yanayodaiwa kuchochea jamii.
Kwa nukuu; 'Wakenya wataleta mapinduzi kwa nchi hii, kama ni kutosha imetosha, tumechoka kama Wakenya, mapinduzi yako na watu! Uhuru uko pamoja na watu! Mapinduzi yako pamoja na watu! Nguvu ya watu! Nguvu ya watu! nguvu ya watu'.
Kesi hiyo itasikilizwa Machi 31, 2016.