Matamshi ya mwanasiasa Suleiman Shahbal kuwa muungano wa Jubilee utashinda katika uchaguzi wa 2017 kwa vyovyote vile yanazidi kuibua hisia mbalimbali mkoani Pwani, na sasa Gavana wa Kaunti ya Kilifi Amoson Kingi anataka achukuliwe hatua.
Katika kikao na wanahabari afisini mwaka siku ya Jumanne, Gavana Kingi alisema tayari amepata kanda ya video inayoonyesha mwanasiasa huyo akisema namna Jubilee itakavyoshinda uchaguzi wa 2017.
Katika kanda hiyo, Suleiman ambaye tayari ametangaza azma yake ya kuwania kiti cha Ugavana wa Kaunti ya Mombasa katika uchaguzi ujao anaonekana akisema kuwa hakuna kitu kitakachozuia mrengo wa Jubilee kushinda uchaguzi huo.
"Safari hii nawambia, tutashinda uchaguzi wa 2017 kwa nguvu, tutaiba, tutashinda kwa mbinu zote,’’ Suleiman anaonekana kwenye kanda hiyo akisema.
Suleiman alikuwa akizungumza siku ya Jumamosi mjini Kilifi katika mkutano uliohudhuriwa na Naibu Rais William Ruto.
Gavana Kingi alisema atawasilisha kanda hiyo kwa idara ya usalama, huku muungano wa Cord ukitafuta ushauri wa kisheria kabla kuchukua hatua.
Kingi vilevile alisema matamshi ya kiongozi huyo yanaashiria kutokuwa maarufu kwa muungano wa Jubilee katika eneo la Pwani.
"Hii ni ishara tosha kuwa Jubilee haina wafuasi Pwani, sasa wanataka kutumia mbinu chafu kupata umaarufu. Hatutawakubalia,’’ alisema Kingi.
Suleiman Shahbal aliwania kiti cha ugavana wa Kaunti ya Mombasa katika uchaguzi uliopita kwa tiketi ya Wiper, lakini alishindwa na Ali Hassan Joho kisha baadaye akahamia mrengo wa Jubilee.
Siku ya Jumamosi alinaswa kwenye kanda ya video akisema namna Jubilee itashinda uchaguzi wa 2017 kwa lazima, matamshi yaliyokashifiwa vikali na Wakenya kwenye mtandao wa kijamii.