Wasimamizi wa sekta ya elimu katika kaunti zote nchini wameagizwa kuwachukulia hatua za kisheria walimu wakuu ambao wataruhusu sherehe za mazishi na sherehe zingine kuandaliwa katika viwanja vya shule zao.
Agizo hilo limetolewa baada ya kubainika kuwa masomo hutatizwa kupitia sherehe hizo ambazo hufanyiwa katika viwanja vya mashule, jambo ambalo sasa limepigwa marufuku nchini
Akizungumza siku ya Alhamisi katika eneo la Riragia eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini, waziri wa elimu nchini Fred Matiang’i aliagiza wasimamizi hao wa sekta ya elimu katika kaunti zote kuchukua sheria dhidi ya mwalimu mkuu ambaye ataruhusu sherehe kufanyiwa katika viwanja vya mashule siku za masomo.
Matiangi alisema masomo ndio msingi wa maisha, huku akisema ni vibaya masomo yanapotatizwa shuleni bila sababu ya kusaidia.
“Naagiza wasimamizi wa sekta ya elimu katika kaunti zote nchini kumchukulia hatua mwalimu mkuu ambaye atavunja sheria ya kupiga marufuku sherehe kufanyiwa katika viwanja vya mashule,” alisema Matiang’i.
Aidha, Matiangi alitoa jibu mbadala kwa sherehe hizo na kusema kuwa zinastahili kufanyiwa katika viwanja vya makanisa.