Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wazazi katika kaunti ya Kisii wamempongeza waziri wa elimu nchini Fred Matiang’i kwa kufutilia mbali hafla zote za mazishi kufanyiwa katika viwanja vya shule.

Hii ni baada ya waziri Fred Matiang’i kusema kuwa hii inafuruga na kuathiri shughuli za masomo shuleni huku akisema watoto wana haki kufunzwa kwa siku tano mfululizo kwa wiki na si siku nne baada ya kubainika siku za Ijumaa mara nyingi viwanja vya shule hutumika kufanya sherehe za mazishi.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Kisii idadi nyingi ya wazazi wakiongozwa na Patrick Onchoke na Hadson Mariita walimpongeza Matiang’i kwa kukataa sherehe hizo kuandaliwa shuleni.

“Tunashukuru waziri Matiang’i kwa kusema hafla za mazishi zisifanyiwe kwa viwanja vya mashule maana watoto wetu walikuwa wanafundishwa kwa siku nne kwa wiki na hiyo ni njia moja ya kuwanyima watoto haki yao katika masomo,” alisema Patrick Onchoke mmoja wa mzazi.

Matiang'i alisema hilo halitakubaliwa kuendelea kamwe huku akisema sherehe hizo zinastahili kufanyiwa katika viwanja vya masoko na katika viwanja vya makanisa ili masomo kutoathiriwa shuleni.

“Tunaona huenda sekta ya elimu italainika katika taifa letu kufuatia jinsi waziri Matiang’i ameanza kufanya mabadiliko na tunamuomba aendelee ili kuinua viwango vya elimu nchini,” alisema Hadson Mariita mzazi.