Waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i amejitokeza kuwaonya vikali walimu wakuu wa shule za umma dhidi yakuwalipisha wanafunzi pesa za mitihani ya kitaifa. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza wakati wa kutangaza rasmi matokeo ya mtihani wa kidato wa KCSE mwaka jana, Matiang'i alisema kuwa wizara yake itachukulia mwalimu yeyote atakayepatikana akiitisha pesa hizo hatua kali za kisheria. 

"Ni wazi kwamba shule inawalipia wanafunzi katika shule za umma pesa za mitihani ya kitaifa na ni jambo la kushangaza kwamba baadhi ya walimu waliitisha pesa za mitihani kutoka kwa wanafunzi mwaka jana ila hiyo ni kinyume na agizo la serikali," alisema Matiang'i. 

Matiang'i aidha alisema kuwa serikali ya kitaifa ilichukua hatua ya kulipa pesa za mitihani ya kitaifa kwa wanafunzi wanaosoma katika shule za umma ili kuwawezesha wanafunzi wanaotoka katika familia maskini kupata nafasi yakufanya mitihani hiyo.

"Siwezi nikaketi kwenye wizara ya elimu huku nikiangalia kuona agizo la serikali likivunjwa kwa maana serikali ilijitolea kuwalipia wanafunzi karo ili kuwawezesha wale wanaotoka katika familia maskini kupata nafasi ya kufanya mitihani ya kitaifa," aliongeza. 

Matiang'i vilevile aliwahimiza wazazi kote nchini kushirikiana na wizara ya elimu kwa kuripoti visa ambapo walimu wakuu watapatikana wakiitisha pesa za mitihani kutoka kwa wanafunzi ili hatua kali kuchukuliwa dhidi ya walimu hao. 

"Ni jambo la mhimu kwa wazazi kushirikiana na maafisa wa wizara ya elimu kwa kuripoti walimu wanaokiuka agizo la serikali, na mimi kama waziri wa elimu sitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu walimu wa aina hiyo," alihoji Matiang'i.