Chuo kikuu cha Garissa kimeanza shughuli ya kusajili watu ambao watashiriki kwenywe mbio za masafa marefu zitakazofanyika mwezi wa Aprili mwaka huu.
Nia na mathumuni ya mbio hizo ni kuleta pamoja watu wa kaunti ya Garissa pamoja na wanafunzi wa chuo hicho, kauli mbiu ikiwa ni kuwakumbuka wanafunzi waliopoteza maisha yao kwenye mkasa uliofanyika Aprili mwaka jana.
Kwenye zoezi hilo, chuo cha Garissa kimepata ufadhili kutoka kwa shirika lisilo la kiserikali, Africa Talent And Change Foundation ambalo linahudumu mjini Garissa.
Akiongea na wanahabari akiwa kwenye chuo hicho, mkurungenzi mtendaji wa shirika hilo Abdi Aziz Mohamed alisema kuwa wamejitolea kuwapa ufadhili chuo hicho ili zoezi liweze kuendelea jinsi ilivyopangwa na kuona watu wengi wakijisajili.
“Tumefadhili zoezi hili ili shughuli zote ziendelee kama ilivyopangwa na tuwe na idadi kubwa ya watu kujitokeza,” alisema Mohamed.
“Kila mtu anaweza akashiriki zoezi hili, wazee, akina mama, waislamu, wakiristo, wanaume na pia wanawake. Ni zoezi huru kabisa,” Alisisitiza Mohamed.
Mohamed aidha aliiomba serikali ya kaunti ya Garissa kuchangia pakubwa katika ufanisi wa shughuli hiyo, na pia ameitaka mashirika mengine yasiyo ya kiserikali kujitolea ili kuusaidia zoezi kuwavutia watu wengi.
“Tunaomba serikali ya kaunti ya Garissa kuchukua pakubwa katika ufanisi wa shughuli hii na pia mashirika mengine yasiyo ya kiserikali yajitolee ili mpango huu mzima uwe bora na kuvutia watu wengi wa kujisajili,” aliongeza Mohamed.
Wote wanaotaka kushiriki zoezi hili wanatakiwa kujisajili ndani ya chuo hicho, huku wakitoa ada ya usajili ya shilingi 500 ambapo usajili wa watu utaendelea hadi Machi 25 mwaka huu.
Ikumbukwe kuwa wanafunzi 148 walipoteza maisha yao Aprili, 2, 2015 wakati wanamgambo wa kundi la Al Shabaab walivamia chuo hicho na kusababisha maafa mengi huku ikiilazimu chuo chenyewe kufungwa kwa muda wa miezi tisa.