Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko, amewataka machifu na manaibu wao kuunda muungano na kutengeza jumuia ya akiba na kukumbatia mbinu za kuwekeza hela na kujiunga na taasisi za kutoa mikopo za kifedha kama mabenki na vyama vya ushirika.
Akiwahutubia siku ya Jumatatu machifu na manaibu wao katika ukumbi wa shule ya upili ya The Star of the Sea kwenye hafla ya kuanzishwa chama za uwekezaji cha viongozi hao, mwakilishi huyo wa wanawake alisema kuwa kwa mda mrefu, viongozi hasa wa mashinani wamekuwa wakijipata katika ugumu wa kuwekeza na kukosa mbinu mwafaka za kuweka akiba ya mapato yao kwa kukosa mwelekeo wa kitaalam.
Bi Mboko aliwakumbusha machifu na manaibu wao na wakazi kwa jumla kuwa tayari wana nafasi katika jamii ya kujiendeleza zaidi kwa kuunda makundi kwa ushirika na kuandikisha Jumuia ambazo zitawapa nafasi ya kutuma maombi ya kupata kandarasi katika serikali za Kaunti na serikali ya taifa ili kuweza kufanikisha maazimio ya uchumi.
Aidha akiongea kwa niaba ya Gavana Ali Joho, Bi Mboko aliongeza kuwa serikali ya kaunti inaweka juhudi ili kuona matatizo yote yanayowakumba wakazi kwenye Kaunti hasa matatizo ya maji ambayo yamekuwa donda dugu.