Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko amesema kuwa mrengo wa Cord utashinda katika uchaguzi mkuu ujao na kuwabandua viongozi waliyoko mamlakani.
Akizungumza katika eneo la Likoni mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Mboko alisema kuwa mrengo wa Cord umejiandaa vyema katika uchaguzi mkuu ujao na watashinda uchaguzi huo, iwapo wizi wa kura utakomeshwa.
Mwakilishi huyo alidai kuwa baadhi ya viongozi walio madarakani hutegemea wizi wa kura kusalia madarakani.
Mboko alisema kuwa mrengo wa Cord utazuru hadi mashinani kuwashawishi wakaazi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo, na kuwaonya dhidi ya kudanganywa na baadhi ya wanasiasa kwa kuwashawishi kifedha ili kuwachagua viongozi wasiofaa kuliongoza taifa hili.
“Tafadhali ndugu zangu tusikubali kudanganywa na baadhi ya viongozi wa kisiasa kwa kuwashawishiwa kifedha na kuwachangua, kwani viongozi hao ni walafi, wafisadi na wanyanyasaji. Kuweni waangalifu ili tubadilishe uongozi wa eneo la Pwani na Kenya kwa jumla,” alisema Mboko.
Mboko aliwarai wakaazi wa eneo la Pwani kujitokeza kwa wingi na kujisajili kama wapiga kura ili kuungana na mrengo wa Cord kuubandua mamlakani mrengo wa Jubilee.
Alisema kuwa mrengo huo umewakandamiza wapwani kwa muda mrefu na wakati umefika sasa wa kuwaondoa uongozini.
Kauli ya Mboko inajiri huku mchakato wa kisiasa ukichukua mkondo mwengine kufuatia kuchipuka kwa viongozi mbalimbali wanaowania nyadhifa za uongozi serikalini.