Mbunge wa Mvita Sharif Nassir amemtaka kiongozi wa waliowengi bungeni Adan Duale na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen kujiuzulu baada ya kutajwa kwenye hati ya kiapo iliowasilishwa na aliyekua Waziri wa Ugatuzi Ann Waiguru.
Kwenye mahojiano na mwahabari huyu siku ya Alhamisi, mbunge huyo alisema kuwa Duale anafaa kujiuzulu mwenyewe kama kiongozi bila ya kulazimishwa, ili kuipa tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC, nafasi ya kuwachunguza yeye na seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, kufuatia kuhusishwa katika sakata ya ufisadi ya NYS.
Aidha, Nassir alisema huo ni mwanzo tu wa kufichuka kwa sakata za ufisadi zinazoendeshwa na walio serikalini, na kuwa mengi yatazidi kudhihirika kwenye siku zijazo.
Itakumbukwa kuwa pia baadhi ya wabunge wa mrengo wa Jubilee, ikiwemo Alfred Keter wa Nandi Hills na Oscar Sudi wa Kapseret waliwataka wawili hao kujiuzulu ili wafanyiwe uchunguzi kuhusiana na sakata hiyo ya shilingi milioni 791 za NYS.