Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua ameahidi kuwa ataendelea kutumikia wananchi wa kaunti yake na kuhakikisha kuwa malengo ya serikali ya ugatuzi unatimizwa.
Mbugua alikuwa akizungumza siku ya Alhamisi katika shule ya msingi ya Kuranga, Wadi ya Murindat kaunti ndogo ya Gilgil ambapo alitoa msaada wa sare zaidi ya 700 kwa wanafunzi a shule hiyo.
Gavana huyo ameelezea kuwa azma yake kuu ni kuhakikisha kila eneo katika kaunti hiyo linapata maendeleo ili kupigana vita dhidi ya ukosefu wa kazi, kuzuka kwa magonjwa, njaa na umaskini.
"Sababu kuu ya kuwa uongozini ni kutumikia wananchi. Hii ndiyo maana tutaendelea kufanya kazi ili kupigana na umaskini na njaa na kuhakikisha malengo yetu ya ugatuzi yanatimizwa," Mbugua alielezea.
Gavana huyo pia ameomba ushirikiano kutoka kwa wananchi ili kuhakikisha kuwa ndoto za wakuu wao watangulizi zinatimia. Mbugua aliambatana na waziri wa elimu wa kaunti hiyo Francis Mathea na waziri wa fedha Ann Njenga miongoni mwa mawaziri wengine na viongozi wengine wa kaunti hiyo.