Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua amewarai wawekezaji kujitokeza na kujenga miradi mbalimbali katika kaunti hiyo ambayo itasaidia kaunti hiyo kuendelea zaidi.
Mbugua pia ameelezea kuwa hatua hiyo itasaidia pakubwa kupunguza idadi kubwa ya watu wasioajiriwa ili wananchi wapate kujikimu mahitaji yao ya kila siku.
Gavana huyo wa Nakuru alikuwa akizungumza siku ya Jumamosi alipokuwa akifungua rasmi tawi la kampuni ya mafuta ya REGNOL OIL katika barabara ya Nakuru-Nairobi.
"Tunafurahia sana kuona wawekezaji wakifungua miradi mbalimbali katika kaunti hii. Tawi hili la mafuta litasaidia wananchi kupata ajira na hata watu wanaosafiri kutoka maeneo mengine kupitia barabara hii watapata kupumzika humu na kushuhudia maendeleo ya kaunti hii," Mbugua alielezea.
Gavana huyo pia amewahakikishia wawekezaji kuwa kaunti yake itakuwa tayari kuwasaidia ili kuhakikisha kuwa malengo yao yanatimizwa.
"Sera yetu kama kaunti ni kuhakikisha miradi mipya zinazoanzishwa zinanawiri kwa haraka iwezekanavyo huku tukiwa na lengo la kuboresha hali ya uchumi na maisha kwa wananchi wetu," Mbugua alielezea.
Mbugua aliambatana na viongozi wengine katika serikali ya kaunti hiyo pamoja na meneja wa kampuni hiyo Abdirizack Aress ambaye pia alishukuru kaunti hiyo kwa kuwapa wakati rahisi katika kujenga tawi hilo.
"Letu ni kushukuru serikali ya Kaunti ya Nakuru kwa kuturuhusu kujenga tawi hili katika eneo hili. Tutazidi kushirikiana na kaunti hii ili kuhakikisha eneo hili linapata kuendelea kwa kasi zaidi," Abdirizack aliongezea.