Mbunge mwakilishi wa akina mama katika kaunti ya Nakuru Mary Mbugua amewataka polisi kuharakisha kuchunguza aliyehusika na mauaji ya msichana mmoja wa miaka 20 mfanyabiashara wa ngono mjini Nakuru wiki jana.
Bi Mbugua alitaja mauaji ya wasichana wanaofanya kazi hiyo kama hujuma, akiwataka polisi kuzuia wimbi hilo la kuanzia mwaka jana.
Marehemu Grace Wangari alipatikana kwenye chumba kimoja cha malazi kwenye hoteli mjini Nakuru, huku mavazi yake yakilowa damu.
Katika mwaka wa 2015, visa kadhaa vya mauaji ya wafanyibiashara wa ngono kuuawa viliripotiwa mjini humo, wakidaiwa kuuawa na mtu asiyejulikana.
“Wafanyibiashara wa ngono hawafai kuuawa kwa kile ambacho wanafanya, kwa sababu ni Wakenya na wanahitaji ulinzi. Tufuate sheria katika kutatua tofauti yetu,” alisema Mbugua.
Babake marehemu Njoroge Kang’au alitaka polisi pia kuharakisha uchunguzi na kuipa familia hiyo haki.
Naye Faith Omari ambaye ni mwanachama katika kikundi cha wafanyikazi hao wa ngono kwa jina Smart Ladies ambapo marehemu alikuwa mwanachama, alitaka polisi kueleza kiini cha mauaji ya wenzao.