Mbunge wa Mavoko Patrick Makau amemkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa madai kuwa aliegemea upande wa kabila mbili katika uteuzi wa mawaziri.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano Kupitia njia ya simu, Makau alidai kuwa kabila mbili ndizo zimemiliki nusu ya wizara zilizotangazwa na rais, jambo ambalo halikufurahisha wengi.
Mbunge huyo alisema kuwa ukabila ndio ufisadi mkubwa na hivyo rais anapaswa kupeana nyadhifa za wizara bila kuegemea upande wowote.
Makau alimkosoa rais kwa kusema ingawaje anaongoza katika vita dhidi ya ufisadi, alionyesha ufisadi mkuu katika uteuzi wa mawaziri.
"Ukabila ndio ufisadi mkubwa ambao tunafaa kumaliza. Ni wazi kuwa rais aliegemea upande wa kabila mbili alipokuwa anawateua mawaziri,” alisema Makau.
Aliongeza, "Kuna makabila mengi nchini ambayo yanahitaji kuwakilishwa na rais angetilia hayo maanani, ili kusawazisha wizara hizo bila ubaguzi.”
Makau alisema kuwa kazi ya rais in kuunganisha kabila zote na itakuwa vigumu kufaulu iwapo ataegemea upande wowote.