Mbunge wa Borabu Ben Momanyi amemtaka kiongozi wa waliowengi kwenye bunge la taifa Aden Duale kumwomba kinara wa Cord Raila Odinga msamaha.
Haya yanajiri baada ya aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi nchini Anne Waiguru kumtaja Duale kama mmojawapo wa maafisa wa serikali wanaodaiwa kuhusika katika sakata ya mamillioni ya pesa katika shirika la huduma kwa vijana nchini la NYS.
Akihutubia mkutano wa hadhara kule Nyansiongo siku ya Alhamisi, mbunge huyo alisema kuwa wakati umefika kwa Duale kumwomba Raila msamaha kwa kumharibia jina.
"Yafaa Duale ajitokeze rasmi na kumwomba Raila msamaha kwa kuwa tayari ametajwa kuhusika kwenye sakata ya uvujaji wa mamillioni ya pesa kutoka kwa shirika la NYS,” alisema Momanyi.
Aliongeza, “Duale alikana madai hayo hapo mwanzoni kwa kusema kuwa muungano wa Cord ulikuwa ukiingiza siasa katika suala hilo, na ndio maana sharti amwombe Raila msamaha."
Momanyi aidha alimshtumu Duale huku akimtaja kama kiongozi kigeugeu anayezungumzia masuala yanayowakumba Wakenya bila ya kuyadadisi, hali aliyosema yafaa kumfanya mbunge huyo wa Garissa mjini kumwomba Raila msamaha.
"Duale ni kiongozi kigeugeu kwa maana hivi maajuzi alikuwa akimtetea vikali Waiguru kuhusiana na sakata hii ya NYS na sasa amegeuka kumtaja Waiguru kama mfisadi baada yake kutajwa kuhusika kwenye sakata hiyo,” alisema Momanyi.
Momanyi vilevile alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kutangaza rasmi ufisadi kama janga la kitaifa ili kuruhusu mashirika ya kimataifa kuingilia kati na kuchunguza donda hilo nchini.
"Wakati umefika kwa Rais Kenyatta kutangaza rasmi kuwa ufisadi umekuwa janga la kitaifa ili kuruhusu mashirika ya kimataifa kuingilia kati, kwa vile mashirika yote ya serikali yanakabiliwa na madai ya ufisadi,” alisema Momanyi.