MCA wa wadi ya Kabazi katika kaunti ya Nakuru Mwangi Waithaka ameitaka serikali ya jimbo hilo kutoa fedha za basari kabla ya muhula wa kwanza wa masomo kung'oa nanga mwaka ujao.
Akiongea na mwandishi huyu Alhamisi, Waithaka alisema wao waliidhinisha kutolewa kwa fedha hizo mwezi Mei 2015, lakini hadi sasa bado serikali ya jimbo haijazituma kwenye shule husika.
Alisema ni jambo la kuhuzunisha kuona serikali hiyo ya kaunti ikiendelea kushikilia fedha hizo kwenye kaunti yake, wakati baadhi ya wazazi wanateseka kutafutia watoto wao karo.
Wito kutoka kwa mwakilishi huyo wa wadi umejiri huku shule zikitarajiwa kufunguliwa katika muda wa wiki moja ijayo.