Makundi ya vijana katika kaunti ya Nakuru sasa yanaitaka serikali ya gavana Kinuthia Mbugua kuwapa asilimia 30% ya zabuni kama inavyotakikana kisheria.
Makundi ya vijana kutoka maeneo bunge ya Molo, Kuresoi Kusini na Kuresoi kaskazini yalidai licha ya rais Uhuru Kenyatta kutilia mkazo hoja ya vijana kutengewa asilimia hiyo ya kandarasi, bado serikali za majimbo zinapuuzilia makundi ya vijana ambayo yametimiza matakwa yote ili kuomba zabuni.
Wakiongea mjini Molo na kuongozwa na mwenyekiti wao Ezekiel Wairobi vijana hao wamesema licha ya vijana kusajili na kuanzisha kampuni bado kandarasi zinatolewa kwa kampuni za watu maarufu na wenye ushawishi mkubwa wa kifedha.
“Tumegundua kwamba baadhi ya viongozi katika bunge la kaunti na serikali ya Nakuru, wamesajilisha kampuni zao, ambazo zinapewa kandarasi hizo. Vijana wanaenda katika ofisi za kaunti na kununua kandarasi hizo kwa shilingi 3,000 lakini wanaishia kuzikosa,” Wairobi alisema.