Hali ya taharuki ilitanda katika eneo la Freehold, viungani mwa mji wa Nakuru siku ya Jumamosi, baada ya miili ya mume na mkewe kupatikana nyumbani mwao.
Miili ya Olivia Osidian na Jack Omondi, ambao walikuwa na watoto wawili, ilipatikana katika chumba chao baada ya majirani kulazimika kutafuta mianya na kupenya chumbani humo, baada ya kushuku kuwa mambo hayakuwa ya kawaida.
Hata hivyo, wanao wawili, wenye umri wa miaka sita na moja na nusu mtawalia, walipatikana wakiwa wazima ndani ya chumba hicho.
Kulinganana majirani, huenda maafa hayo yalitokana na mzozano kuhusu pesa, ambao unadaiwa kushuhudiwa kwa muda kati yao.
“Hawa wamekuwa wakigombana kila kuchao kuhusu pesa na tunafikiria ndicho kiini cha maafa hayo,” alisema mmoja wa majirani.
Akidhibitisha kisa hicho, Naibu OCPD wa Nakuru, Janet Wasige, alisema kuwa huenda maafa hayo yalitekelezwa siku ya Jumatano kwani miili ya wawili hao tayari ilikuwa imeanza kutoa uvundo.
Uchunguzi wa tukio hilo tayari umenzishwa huku miili ya wawili hao ikipelekwa katika ufuo wa Hospitali kuu ya Nakuru.