Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Kisauni Julius Kavita amesema kwamba kuna haja ya watoto kupelekwa shuleni ili kuepukana na visa vya dhuluma za kimapenzi.

Akiongea katika kongamano la kiusalama na wadau mbali mbali eneo la Kisauni mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Kavita alisema kwamba visa hivyo vimechangiwa pakubwa na wazazi kukosa kuwajibikia majukumu hayo ya kuwapa msingi bora wa elimu watoto wao.

Kulingana na Kavita, kukithiri kwa taasubi ya kiume, mila na tamaduni zilizopitwa na wakati ndizo zinachangia kukithiri kwa visa hivyo, na akasema kwamba ni lazima kwa wazazi kukoma kuwanyanyasa watoto wao haki zao za kimsingi.

"Hii kushiriki sana mila na tamaduni zilizopitwa na wakati ndio zinachangia kukithiri kwa visa vya ubakaji katika jamii, na kwa sababu ya kuamini sana mila hii maneno inaishia kinyumbani na hiyo ni hatari kubwa sana kwa mtoto wa kike kwa sababu hatapata haki zake kikamilifu, na ndio maana mimi nawaomba wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni na kupata msingi bora wa elimu kupunguza visa hivi," alisema Kavita.

Wakati uo huo, alitoa changamoto kwa maafisa wa usalama kuhakikisha kwamba wanashirikiana na viongozi wa nyumba kumi, askari jamii na maafisa tawala kuwakamata watoto wote wanaoranda randa mitaani ili kuwapeleka shuleni na wazazi wao kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Kauli yake hii ilijiri baada ya Kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa kuagiza kuondolewa kwa vibanda vya wafanyibiashara wanaoendeleza shughuli zao karibu na malango ya shule kwani wanachangia kutoa ushawishi kwa baadhi ya wanafunzi wa kike na kupelekea kuwadhulumu kimapenzi.