Share news tips with us here at Hivisasa

Mtu mmoja ameripotiwa kufariki huku wengine wawili wakijeruhiwa baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba usiku wa kuamkia siku ya Jumatano.

Kulingana na ripoti zilizotolewa na Shirika la Msalaba Mwekundu katika Kaunti ya Mombasa, ukuta huo uliporomoka kufuatia mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha pamoja na upepo mkali.

Tukio hilo lilitokea katika mtaa wa Moroto, eneo la Tudor, mjini Mombasa, huku maafisa wa shirika hilo wakizuru nyanjani kuwaelimisha wakazi jinsi ya kuepukana na majanga sambamba na kuwashauri kuhamia maeneo ya juu.

Wakati huo uo, wakazi zaidi ya 11 wameokolewa huko Mikindani eneo Bunge la Jomvu, baada ya nyumba yao kuporomoka kutokana na mvua kumbwa iliyonyesha usiku.

Hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa katika mkasa huo.

Shirika la Msalaba Mwekundu kaunti ya Mombasa limewashauri wakazi kuwa waangalifu hasa wakati huu wa msimu wa mvua ili kuepukana na majanga huku wakazi wanaoishi maeneo ya mabonde wakishinikizwa kuhamia maeneo ya juu.