Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Baada ya Katibu katika Wizara ya Uchukuzi na Miundo Msingi nchini John Mosonik kukutana na wasimamizi wa shirika la huduma za feri nchini na kujadili tatizo linalozikumba feri hizo, wakazi wameonekana kumkosoa katibu huyo.

Wakazi hao walidai kwamba hatua aliyochukua katibu huyo ni kinyume na jinsi wakazi walivyotarajia kwani walitarajia kupata ripoti ya uchunguzi wa usimamizi wa shirika hilo.

Wakizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Ijumaa, wakazi hao wakiongozwa na Khamis Mwadziga walisema kwamba hali ya msongamano katika kivuko cha feri cha Likoni bado inazidi kushuhudiwa licha ya viongozi wa serikali kudai kuimarisha hali hiyo katika kivuko hicho.

“Tunashangazwa na Katibu katika Wizara ya Uchukuzi na miundo msingi Mhandisi John Mosonik kwa kushindwa kuyaangazia vyema masaibu ya kivuko cha feri, na kutuambia kuwa atatuma maafisa wa wizara yake kuja kufanya uchunguzi. Sisi tunataka usimamizi wa shirika la feri kufanyiwa mabadiliko,” alisema Mwadziga.

Aidha, wakazi hao walipendekeza kuvunjiliwa mbali kwa bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo, na kubuniwa bodi nyingine huku wakishinikiza kufutwa kazi kwa Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Hassan Musa na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi James Fondo kwa madai ya kuzembea kazini.

Wakati uo huo, wakazi hao waliukosoa mpango wa serikali ya Kaunti ya Mombasa ya kutaka kuchukua jukumu la kusimamia shirika hilo, wakisema kwamba kuna baadhi ya viongozi waliyo na njama potovu ya kuhujumu fedha za umma kupitia mpango huo.

Mchakato huyo wa usimamizi wa shirika la huduma za feri umejiri siku chache baada ya kushuhudiwa msongamano wa abiri wakati wa kuabiri feri na kusababisha majeruhi ya zaidi ya watu 11.