Share news tips with us here at Hivisasa

Wahudumu wa maduka yakuuza filamu mjini Nakuru wameonywa dhidi ya kuwauzia watoto na wanafunzi filamu za ngono.

Naibu afisa mkuu wa watoto katika kaunti ya Nakuru Stella Chelegat amesema kuwa baadhi ya maduka ya kuuza filamu mjini Nakuru huwauzia watoto filamu za ngono.

Chelegat alisema kuwa idara ya watoto itashirikiana na polisi kufunga maduka kama hayo.

Akiongea siku ya Jumanne mjini Nakuru, wakati wa shughuli ya uhamasisho kuhusu athari za filamu za ngono kwa watoto, Chelagat alisema kuwa maduka mengi na vituo vya kuonyesha filamu havizingatii umri wa wanafunzi kabla ya kuwauzia filamu hizo.

“Kuna maduka mengi sana ya kuuza filamu mjini Nakuru yanayowauzia watoto walio chini ya umri wa miaka 18 filamu za ngono. Hiyo ni kuvunja sheria na pia haki ya mtoto,” alisema Chelagat.

Aliongeza, “Kabla ya muuzaji kumuuzia yeyote filamu ya ngono, ni lazima amuulize kama ametimiza miaka 18 na iwapo hajatimiza, basi hafai kuuziwa filamu hizo.”

Chelagat aidha aliwataka wazazi kuchunguza aina ya filamu watoto wao wanazotazama ili kuwaepusha na tabia ya kutazama filamu zisizofaa.

Alisema kuwa idara ya watoto itashirikiana na polisi kuendesha msako wa ghafla katika maduka yote ya kuuzia filamu ili kuwanasa wanaouza ama kuonyesha filamu hizo.