Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Idara ya afya na usafi wa umma katika Kaunti ya Nakuru imeanzisha msako dhidi ya hoteli zinazokikuka sheria za afya kama njia moja ya kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu katika eneo hilo.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, msimamizi mkuu wa maswala ya afya katika Kaunti ya Nakuru Samuel King’ori alisema kuwa kufikia sasa, maeneo tisa ya kuuziwa chakula katika eneo la Kikopey lenye umaarufu wa kuuza nyama choma huko Gilgil yamefungwa.

King’ori alisema hoteli hizo zimefungwa kutokana na uchafu mwingi huku hoteli zingine mbili zilizo kwenye barabara ya Nakuru kuelekea Nairobi zikipewa ilani.

Afisa huyo alisema kuwa wanafanya kila wawezavyo ili kuweza kuudhibiti ugonjwa huo ambao umeonekana kulemea maeneo tofauti ya Gilgil.

“Uchafu mwingi ulioko katika vitongoji duni vya Gilgil haswa eneo la Kasarani ndio ambao umechangia pakubwa kuzuka kwa ugonjwa huu hatari wa kipindupindu,” alisema King’ori.