Mshukiwa wa mauwaji ya Sheikh Mohamed Idris ameshikilia msimamo wake wa kukanusha kuhusika katika mauwaji hayo mnamo mwaka wa 2014.
Mohaned Soud alisisitiza kuwa hakuhusika na mauwaji hayo, bali alijipata katika mikono ya polisi huku wakimuhusisha na mauwaji hayo ambayo hayatambui kamwe.
Soud aliwalaumu maafisa wa usalama kwa kumuhusisha na umiliki wa bunduki na kilipuzi, ikizingatiwa hana ujuzi wa kutumia silaha hizo hata kidogo.
Aidha, aliongeza kuwa maafisa wa usalama walimfunga kitambaa cha macho na kumzungusha kwa vituo kadha vya polisi kwa takrbani masaa manane, na kumwacha bila chakula, jambo alililitaja kama kinyume cha haki za binadamu.
Soud alsisitiza kuwa hakuwa na chuki wala misimamo tofauti ya kidini na marehemu Idris, na kuiambia mahakama kuwa walikuwa marafiki wa dhati.
Soud aliyasema haya alipokuwa akitoa ushahidi wake katika mahakama kuu ya Mombasa siku ya Jumatatu.
Mnamo Juni 10,2014, Mohamed Soud anadaiwa kuhusika katika mauwaji ya marehemu Sheikh Mohamed Idris katika eneo la Likoni.