Hadi kufikia sasa jamaa wawili kati ya wanne kutoka eneo la majengo wanaohusishwa na shutuma za ugaidi wameweza kukamatwa na kufikishwa katika mahakama ya mjini Mombasa.
Mahmoud Salim Mohammed alifikishwa mahakani siku ya Jumatatu baada ya kujisalimisha kwa maafisa wa polisi mjini Malindi siku ya Jumanne kufuatia kuchapishwa kwa picha yake katika vyombo vya habari kama mmoja kati ya wanaosakwa na maafisa kutoka kitengo cha kupambana na ugaidi.
Mahmoud, anayedaiwa kupokea mafunzo kutoka kwa kundi la Al shabaab nchini Somalia, alijisalimisha kwa polisi mjini malindi baada ya picha yake kuangaziwa katika vyombo vya habari na kuhusishwa na ugaidi.
Mshukiwa huyo alifikishwa mahakamani baada ya msako wa polisi uliopelekea kukamatwa kwa bunduki aina ya M4 na G3 pamoja na risasi 345 siku ya Jumatatu katika eneo la majengo Kaunti ya Mombasa.
Vifaa vingine vilivyonaswa na maafisa wa polisi ni pamoja na simu za mkononi kumi na tano na kemikali inayodaiwa kutumika kutengeneza vilipuzi.
Mshukiwa huyo atasalia kizuizini kwa siku 30 hadi uchunguzi dhidi yake kukamilika.