Shee Mohamed Kale, mshukiwa wa ugaidi, atazuiliwa korokoroni kwa siku 14 huku uchunguzi dhidi yake ukiendelea.
Hii ni baada ya afisa wa upelelezi Fancy Sang, kuwasilisha ombi mahakani kuomba muda zaidi wa kufanya uchunguzi wa madai hayo.
Mwendesha mashtaka Eugine Wangila, aliiambia mahakama ya Mombasa siku ya Jumanne kuwa wanataka kumuhoji mshukiwa huyo pamoja na marafiki wake wa karibu kuhusiana na madai hayo ya ugaidi.
Aidha, alisema kuwa wanataka kuchunguza simu ya mshukiwa huyo katika kituo kinacho chunguza matukio ya uhalifu jijini Nairobi.
Hakimu katika Mahakama ya Mombasa, Richard Odenyo alikubali ombi hilo na kuagiza mshukiwa huyo kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Central.
Mshukiwa Shuyo alitiwa mbaroni siku ya Jumatatu katika eneo la Witu huko Kaloleni, na kuhusishwa na kilipuzi kilichowauwa maafisa sita wa polisi tawala katika eneo la Milimani huko Lamu, mnamo Januari 26, 2016.
Kesi hiyo itatajwa Machi 8, 2016.