Share news tips with us here at Hivisasa

Visa vya mauaji ya kiholela vinazidi kushuhudiwa katika mji wa Nakuru, huku polisi wakipata mwili wa msichana mmoja mwenye umri wa miaka 19 siku ya Jumapili, ambaye alikuwa ameripotiwa kupotea.

Marehemu anasemekana kutoka nyumbani kwao katika mtaa wa Pyrethrum viungani mwa mji wa Nakuru Jumatano akienda kutengeza nyweli, lakini hakurudi nyumbani.

Kulingana na wazazi wa msichana huyo, marehemu alikuwa akijitayarisha kujiunga na taasisi ya mafunzo ya Sigalagala mjini Kakamega Jumatatu.

Kulingana na naibu OCPD wa Nakuru Janet Wasike, polisi walishirikiana na familia ya marehemu kumtafuta aliporipotiwa kupotea, lakini wakapata ameuawa na mwili wake kutupwa katika shamba moja lililo karibu na gereza kuu la serikali mjini Nakuru.

“Msichana huyo alikuwa ameripotiwa kupotea alipoenda kusuka nywele katika mtaa wa Bondeni, lakini akakosa kurejea nyumbani,” alisema Wasike.

Wasike alisema marehemu alikuwa na majeraha ya kugongwa kwenye kichwa, dhihirisho kwamba huenda aliuawa na kisha kutupwa shambani humo na kwamba polisi wanatafuta washukiwa wa mauaji hayo.

“Mwili wake umepelekwa katika ufuo wa hospitali ya kaunti ya Nakuru,” alisema Wasike.

Hayo yanajiri siku kadhaa baada ya msichana mwingine anayejihusisha na ukahaba kuawa katika mji huo wa Nakuru.