Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakaazi wa mitaa iliyo kando ya barabara kuu ya Nakuru-Nyahururu wameonywa dhidi ya kuyauza mashamba yao kiholela.

Kulingana na mwaniaji wa kiti cha eneo bunge la Bahati Peter Nderitu, wakazi wengi wameanza kuyauza mashamba yao kwa wawekezaji kutoka nje.

Akizungumza Maili Sita Jumapili, Nderitu alisema kuwa kutokana na kuimarika kwa biashara katika barabara hiyo pamoja na ongezeko la watu,wawekezaji wamevamia maeneo hayo kwa nia ya kununua mashamba kwa bei nafuu.

“Hii barabara imeanza kuandikisha ukuaji mkubwa sana wa biashara na kila mahali ukipita utaona watu wameweka vibao vya kuyauza mashamba yao na mimi nataka kuwatahadharisha na tabia hiyo kwa kuwa sio nzuri,” alisema Nderitu.

“Tusikimbilie kuyauza mashamba kwa bei duni halafu baadaye tuje tujute.Ni vyema tuwekeze katika mashamba hayo sisi wenyewe hata kama ni kujenga majumba halafu tuyakodishe kwa watu,” aliongeza.

Kutokana na kukarabatiwa kwa barabara hiyo kumeshuhudiwa ujenzi wa majumba ya kifahari jambo ambalo linawavutia wawekezaji wengi.

Nderitu aliwaria wamiliki wa mashamba kutokuwa na haraka ya kuyauza kwani wakati mwafaka utafika ambapo watayauza mashamba hayo kwa bei nzuri kuliko ya sasa.

“Itafika wakati hawa watu wa kununua mashamba watakuja kuwatafuta wenyewe na watanunua na bei mtakayosema kwa hivyo tusiwe na njaa sana ya kuuza mashamba kwa bei duni,” akasama.