Share news tips with us here at Hivisasa

Zaidi ya wabunge 10 waasi wa chama cha ODM katika eneo la Pwani wamemtangaza mbunge wa Kilifi Kaskazini, Gideon Mung’aro, kama kiongozi wa kisiasa atakaye waongoza wakaazi wa Pwani katika uchaguzi wa 2017.

Wakiongozwa wa mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Kwale Zainab Chidzuga, wabunge hao walisema kuwa wakati umefika kwa wakaazi wa Pwani kuzungumza lugha moja katika uchaguzi ili matakwa yao yaweze kuaangaziwa na serikali.

Wakizungumza mjini Malindi siku ya Jumamosi katika kampeni za kumpigia debe mwaniaji wa ubunge wa Malindi kwa tiketi ya mrengo wa Jubilee, Philip Charo, wabunge hao miongoni mwao Khatib Mwashetani wa Lunga Lunga, Peter Shehe wa Ganze, Mustapha Idi wa Kilifi Kusini, Gunga Mwinga wa kaloleni pamoja na James Kamote wa Rabai, walimtaja Mung’aro kama kiongozi mwenye uwezo wa kuwaunganisha Wapwani pamoja.

Wabunge hao aidha walisema kuwa siku za hivi karibuni watatangaza kuvihama vyama vyao rasmi, na kujiunga na chama kipya cha Jubilee, ili waweze kufanya kazi na serikali kwa lengo la kuhakikisha kuwa matakwa ya wakaazi wa Pwani yanaskizwa na kutekelezwa.

Kwa upande wake, mbunge wa Kilifi Kaskazini, Gideon Mung’aro, aliwarai wakaazi wa Malindi kumpigia kura Philip Charo wa Jubilee katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi, huku akimtaja kama mtu wa pekee atakaye waletea wenyeji miradi ya maendeleo.