Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwenyekiti wa mamlaka ya kudhibiti utumizi wa mihadarati na pombe (Nacada) John Mututho amewaonya vijana dhidi ya kujihusisha na pombe haramu na madawa ya kulevya haswa tunapokaribia msimu wa krismasi.

Katika mahojiano kwa njia ya simu na mwandishi huyu jumamosi, Mututho aliwashauri vijana kutafakari kuhusiana na maisha yao ya siku za baadaye na kuchukua msimamo dhabiti akisema uraibu wa madawa ya kulevya ni donda sugu.

Alikariri kwamba badala ya kutumia mihadarati na pombe, vijana wanaweza kujiunga katika makundi ambayo yatawasadia kujiendeleza maishani.

“Badala ya kunywa pombe na kutumia mihadarati, vijana wanafaa kujiunga pamoja ili kufanya mambo yatakayowasaidia. Vijana hawafai kutumia pombe na mihadarati kwa sababu ukianza wakati huu, maisha yako ya siku za usoni yataharibika na hautaweze kujizuia dhidi ya utumizi wa mihadarati na pombe mbeleni,” alisema Mututho.

Kwa mujibu wa mweneyekit huyo, utumizi wa mihadarati waweza kufanya mtu kuwa mfungwa huku akiwashauri watu, haswaa vijana ambao wamejaribu kutumia mihadarati, kukoma kabla hawajapata madhara ambayo yatawachukua muda mwingi na fedha kujiepusha nayo.

“Huenda ukakosa kujizuia dhidi ya kutumia dawa za kulevya na pombe na pia labda huenda ukakosa kusaidiwa kuachana na dawa hizo pamoja na pombe. Wale ambao wameonja pombe kwa mara ya kwanza, nawasihi msijaribu kwa mara ya pili na ya tatu. Dawa aina ya heroine humwadhiri mtu kabisa baada ya kuitumia mara tatu. Pombe pia inaweza kumwadhiri mtu baada ya kuitumia mara mbili,” alidokeza Mututho.

Matamshi yake yanajiri siku chache baada ya waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery kuagiza kufungwa kwa kampuni mia moja kumi na tano za kutengeneza vileo kwa kutozingatia kanuni zilizowekwa.