Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Watu walio na shida ya macho kutoka kaunti ndogo za Manga, Borabu na Masaba hatimaye wamepata sababu ya kutabasamu baada ya madaktari ambao ni wenyeji kaunti ya Nyamira na wanafanya kazi Nairobi kuanza kuwatibu walio na shida.

Kulingana na Dkt Bonface Maisiba, shughuli hiyo ni ya kujitolea kwa muungano wa madaktari wa Gusii kutoka Nairobi na inatarajiwa kuchukua takriban wiki mbili, huku akiwahimiza watu wengi kujitokeza ili kupimwa.

“Sisi ni madaktari wenye ujuzi wa magonjwa ya macho, tunaojitolea kuwapima na kuwapa matibabu watu walio na shida ya macho kwenye eneo la Manga, Masaba na Borabu huku tukiwalenga watu wasio na uwezo wa kuona na wale wasioona vizuri ili tuwape matibabu,” alisema Maisiba.

Maisiba aliongeza kuwa watu wengi hulazimika kusafiri mbali ili kupokea matibabu, akisisitiza kuwa shughuli hiyo itawafaa sana.

“Ni jambo la kushangaza kuwa watu wetu hulazimika kwenda Sabatia, Kijabe na Kikuyu ili kupokea matibabu ya macho kwa kuwa hatuna wataalamu wa magonjwa ya macho Nyamira, hata hivyo watakaopatikana na matatizo ya macho watapewa matibabu,” alisema Maisiba.

Akizungumzia swala la serikali ya kaunti hiyo kushirikiana na muungano wa madaktari hao, Maisiba alisema kuwa yafaa serikali ishirikiane na muungano huo wa madaktari mara kwa mara ili kufanya kliniki kama hizo.

"Itakuwa vizuri iwapo serikali ya kaunti ya Nyamira itashirikiana nasi kufanya kliniki kama hizi mara kwa mara kwa kuwa hatuwezi kufanya kliniki hizi sisi pekee,” alisihi Maisiba.