Share news tips with us here at Hivisasa

Mvulana wa miaka kumi aliaga dunia baada ya kutumbukia katika Mto wa Katine, katika kata ya Tala, kaunti ndogo ya Matungulu.

Akidhibitisha kisa hicho, chifu wa kata ya Tala, Pius Nzioka, alisema kuwa kijana huyo alikua ametoka sokoni akielekea nyumbani, na alipokua akivuka mto huo, alibebwa na maji na kuaga dunia.

Aidha, chifu huyo alielezea kuwa kutokana na mto huo kujaa maji, wazazi wanapaswa kushauri wanao kutumia vivukio vya daraja ili kuepuka kufa maji.

“Mto huo umefurika kutokana na mvua nyingi inayoendelea kushuhudiwa na sio hatari kwa watoto tu bali pia kwa watu wazima,” alisema Nzioka.

Aliongeza, "Ni vyema watu kutumia daraja kuvuka mito kwa ajili ya usalama wao, hata kama daraja zenyewe zipo mbali, kwani inasikitisha kupata habari za watoto kufa maji kila uchao.”

Vilevile, Nzioka aliwakosoa wazazi kwa kutowachunga watoto wao ipasavyo hasaa msimu huu wa mvua.

Mwili wa mvulana huyo unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti ya Hospitali ya Kangundo Level Four.