Baada ya shule nyingi za umma kutoka Keroka kutofanya vyema kwenye mtihani wa kitaifa wa KCPE mwaka jana, mwakilishi wa Nyasiongo, Jackson Mogusu, amefanya kikao cha washikadau ili kujadili jinsi ya kupata suluhu la suala hilo.
Akihutubu katika Shule ya msingi ya Gesebei kule Nyansiongo siku ya Jumatatu, Mogusu aliwahimiza wazazi na walezi kutekeleza majukumu yao bila ya kuingilia majukumu ya walimu.
Alisema kuwa hatua hiyo itahakikisha viwango vya elimu vinaimarika katika eneo hilo.
"Eneo hili limekuwa likifanya vibaya kwenye mitihani ya kitaifa na hilo sio jambo la kutia moyo. Ndio maana nataka kuwahimiza wazazi na walimu kutekeleza majukumu yao bila ya muingiliano wa aina yeyote ule, kwa kuwa hatuwezi kamwe kuimarisha viwango vya elimu iwapo kila kuchao kazi yetu itakuwa ya kurushiana lawana," alisema Mogusu.
Mogusu aidha aliwapa walimu changamoto kutia bidii zaidi wakati wanapo andaa wanafunzi kwa mitihani ya kitaifa, huku akiwahimiza wazazi kuruhusu wanao kuhudhuria shule kama inavyofaa.
Mwakilishi huyo alisema kuwa ripoti zimekuwa zikionyesha kuwa idadi kubwa ya wazazi imekuwa ikiwalazimu wanao kukaa nyumbani ili kuwasaidia kufanya kazi za nyumbani.
"Nimekuwa nikipokea ripoti kwamba kuna wazazi wanao ingililia usimamizi wa shule na hilo halifai kwa kuwa iwapo kuna jambo linaloibua utata, kuna wawakilishi wa wazazi wanao stahili kusuluhisha utata huo kwa ushirikiano na walimu. Walimu pia sharti wawajibike kazini ili kuimarisha viwango vya elimu maana hatutaki kuona matokeo mabaya kwenye mitihani ya kitaifa kama ilivyokuwa mwaka jana," aliongezea Mogusu.