Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi wa wadi ya Shanzu Maimuna Salim Mwawasi siku ya Jumatatu alifikishwa katika mahakama ya Mombasa kujibu mashtaka ya ufisadi dhidi yake.

Mahakama ilifahamishwa kuwa mnamo tarehe 16 mwezi Julai mwaka huu, Maimuna aliitisha hongo ya shilingi laki tano kutoka kwa Morin Leah Aketch ili atoe msaada wake katika kutatua mzozo wa ardhi baina yake na serikali ya kaunti.

Aidha, mwanasiasa huyo alikabiliwa na mashtaka mengine ya kuwatishia maafisa kutoka kitengo cha kupambana na ufisadi walioongozwa na Alfred Mwachugha, sawia na madai ya kuchochea wananchi wachome gari la maafisa hao waliokuwa wakifanya uchunguzi dhidi yake.

Maimuna alishtakiwa pamoja na Christopher Karisa, aliyedaiwa kupokea hongo ya shilingi laki tano kwa niaba yake.

Cheti cha kukamatwa kwa Karisa kilitolewa na hakimu Richard Odenyo baada ya mshukiwa huyo kudinda kufika mahakamani.

Maimuna alikanusha mashtaka yote na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki tatu pamoja na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.

Kesi hii itaskizwa mnamo tarehe 15 mwezi Januari mwaka ujao.

Wakati huo huo katika mahakama hiyo ya mombasa, vijana saba kutoka eneo la Old Town jijini Mombasa wanakabiliwa na mashtaka ya kunuia kutekeleza uhalifu baada ya kupatikana na silaha hatari vikiwemo visu na vyuma.

Aidha, vijana hao wanakabiliwa na mashtaka mengine ya kupatikana na bidhaa zilizokisiwa kuwa za wizi ikiwemo kipakatalishi na nyaya za stima.

Abdul kadir, Abdalla Hamisi, Hamisi Hassan, Kelvin Osobo, Abdulmajid Swaleh, Ahmed Mohsen na Ismael Ahmed walikanusha mashtaka hayo na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki moja kila mmoja pamoja na msimazi wa kiasi sawa na hicho.

Kesi hiyo itaskizwa mnamo tarehe tatu mwezi Februari mwaka ujao.