Mwalimu mkuu wa shule ya Nyakiambi eneo la Elburgon amepewa wiki mbili kutoa ripoti ya ukaguzi wa hesabu kwa afisi ya wazazi na maafisa wa elimu katika kaunti ndogo ya Molo.
Haya ni kwa mujibu wa maafikiano ya kikao cha ghafla na wazazi kilichofanyika Jumatatu shuleni humo.
Hatua hiyo imetokana na maandamano ya wazazi waliokuwa wakipinga swala la mwalimu mkuu huyo la kuwarudisha nyumbani wanafunzi kwa kutolipa shilingi 200 zinazodaiwa kuwa za ziara ya walimu eneo la Pwani.
Wakati uo huo mwalimu mmoja chini ya kamati ya shule hiyo PTA aliachishwa kazi ghafla wakati wa kikao hicho kwa kile kinachodaiwa kuwa aliwatusi wazazi wakati wa maandamano hayo.
Hata hivyo maafisa wa elimu kutoka jimbo ndogo la Molo waliohudhuria kikao hicho wameapa kuchunguza kesi hiyo na kuchukua hatua ya haraka kulingana na mtokeo ya uchunguzi.
Ikumbukwe mwalimu huyo mkuu Allan Mbugua anadaiwa kuitisha hela hizo bila makubalianio kati yake na wazazi japo alikana madai hayo akihojiwa na vyombo vya habari na kudai kuwa aliwahusisha wazazi 120 katika kikao cha mwisho shuleni humo mnamo mwaka jana baada ya matokeo ya mtihani wa KCPE kutangazwa.