Maafisa wa elimu kutoka eneo la Njoro kaunti ya Nakuru, wametakiwa kuchunguza kiini cha matokeo mabaya ya mitihani ya kitaifa kwenye shule ya msingi ya Makutano iliyo eneo la Mau Narok.
Wakiongea na wanahabari baada ya mkutano uliovutia hisia kali Jumatatu, wazazi wenye wanafunzi shuleni humo walisema inahofisha kuona matokeo mabaya ya elimu shuleni humo kila mwaka.
Wazazi hao walisema wengine wao wamelazimika kuhamisha watoto kutoka shuleni humo hadi shule zingine kutokana na kudorora kwa elimu katika shule ya Makutano.
Katika mtihani wa KCPE mwaka wa 2015, shule hiyo ilisajili wanafunzi 17 kufanya mtihani huo, ambapo mwanafunzi bora zaidi alipata alama 309, huku shule hiyo ikiwa na jumla ya wanafunzi 230 pekee.
Wazazi hao wakiongozwa na Samwel Gitonga Ndegwa, walisema kwamba uongozi mbaya ndio unaadhiri matokeo ya wanafunzi wao, huku mwalimu mkuu akipuuzilia wito wao kufanya mkutano wa majadiliano.
“Mwalimu mkuu pia hukosa kufika darasani bila ya sababu zozote. Tunafahamishwa na ofisi ya elimu eneo hili kwamba tayari Mwalimu huyo ameomba uhamisho kutoka shule hii,” Peter Kuria Gachagua alisema.
Afisa msimamizi wa maswala ya uajiri kwenye kaunti ndogo ya Njoro Nancy Muveri alikiri kwamba shule nyingi za eneo hilo hazina waalimu wa kutosha lakini wanafanya kila jambo kutatua tatizo hilo.
“Tumekabidhi tatizo hilo tume ya TSC, na tunaamini kwamba hivi karibuni litatatuliwa,” Muveri alisema.
Mwalimu wa shule hiyo hata hivyo alipuuza madai ya wazazi hao.